Skip to main content

FAHAMU KILA KITU KUHUSU MAGONJWA YA MOYO


LEO tutaelezea kwa kina chanzo cha magonjwa ya moyo ambayo husumbua watu wengi. Chanzo kikubwa ni watu kutozingatia kanuni za ulaji bora, ni moja ya mambo yanayoongeza uwezekano wa mtu kupata magonjwa ya moyo. Kwa mfano, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi nyingi na lehemu nyingi, huku ulaji wa mbogamboga na matunda ukiwa ni wa kiwango cha chini, huongeza uwezekano wa kupatwa na magonjwa ya moyo.

Lakini pia hali ya kuwa na uzito uliozidi kiasi au kuwa na unene uliopitiliza pamoja na kutofanya mazoezi ya mwili na viungo mara kwa mara, huchochea uwezekano wa mtu kukumbwa na magonjwa ya moyo. Wakati mwingine magonjwa ya moyo huweza kutokana na historia ya ugonjwa huo katika familia. Umri unapozidi miaka 50 kuna uwezekano pia wa kupatwa na magonjwa haya ya moyo, huku wanaume wakiwa kwenye hatari zaidi ya kupatwa na tatizo hili mapema zaidi ikilinganishwa na wanawake.

Magonjwa ya moyo huanza kumwandama mtu pale mambo fulani yanaposababisha sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu kuharibiwa. Mambo hayo ni pamoja na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha aina fulani za mafuta na lehemu katika damu.
Hali hiyo inapompata mtu, mishipa ndani ya moyo huweza kufungamana kwa mafuta, hivyo kuleta Mshtuko wa Moyo kitaalamu Heart Attack) au kupooza kwa maana ya kiharusi, yaani Stroke. Aidha, ongezeko la lehemu huongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
Kiujumla, wingi wa lehemu unakadiriwa kusababisha vifo vya watu takriban milioni 2.6 duniani kila mwaka.

Kuwepo kwa sukari nyingi katika damu, husababisha ugonjwa wa Kisukari, ambao unamweka mtu katika hatari ya kupata ugonjwa wa Moyo au kupooza au kiharusi mara mbili zaidi ya asiye na Kisukari. Aidha, kuwa na sukari nyingi kwenye damu kwa muda mrefu, husababisha kuganda kwa mafuta kwenye mirija ya damu. Kuganda huku kunaweza sababisha kupungua kwa mtiririko wa damu kwenye mishipa.
Shinikizo Kubwa la Damu, maana yake ni kwamba moyo unalazimika kusukuma damu kwa nguvu ili kutosheleza mahitaji ya mwili. Kuulazimisha moyo kufanya kazi kuliko kawaida yake, kunasababisha moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure).

Uvutaji wa sigara au utumiaji wa tumbaku kwa kutafuna au kunusa (ugoro), husababisha pia sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu kuharibiwa, hivyo kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo. Kemikali zinazopatikana kwenye tumbaku, huweza kuharibu seli za damu.
Uharibifu huo wa seli, huingilia muundo na utendaji mzuri wa mishipa ya damu. Aidha, kuharibika kwa mishipa ya damu, kunachochea mafuta kuganda kwenye mishipa ya damu (Atheroskerosisi). Unywaji pombe kupita kiasi na utumiaji wa dawa za kulevya ni hatari tena kwa hili. Unywaji pombe mara kwa mara huongeza uzito wa mwili, hali inayoweza kusababisha Shinikizo la Damu kupanda.


Aidha, pombe na dawa za kulevya hudhoofisha misuli ya moyo na mishipa ya damu. Misuli na mishipa ya damu ya moyo ikishadhoofika, huweza kusababisha moyo kutofanya kazi katika ubora wake (Heart Failure). Lakini pia, ikitokea mishipa ya damu ikaharibiwa, mafuta mwilini hujikusanya katika sehemu ya mishipa iliyoharibiwa, hivyo kutengeneza utando wa mafuta (plaque).
Kadri muda unavyoendelea ndivyo mafuta haya yanavyozidi kujijenga katika sehemu hiyo hadi kufanya mishipa hiyo kuwa myembamba, hivyo kupunguza kiasi cha damu kinachobeba hewa ya oksijeni na virutubishi kwenda kwenye misuli ya moyo.
Kitendo hicho kitaalamu, huitwa Atherosklerosisi, ikimaanisha kukakamaa kwa mishipa ya ateri kutokana na mkusanyiko wa mafuta ndani ya ateri.
 
Hatimaye sehemu hiyo ikipasuka, sehemu ya seli za damu zinazoitwa pleteleti za damu (chembe ndogo mviringo ambazo zinahusika na kuganda kwa damu) ambazo husaidia mwili kuponya kidonda, hujigandisha kwenye mpasuko, hivyo kuanza kujikusanya.

Hali hii huongeza mkusanyiko, hivyo kuendelea kufanya mishipa hiyo kuwa myembamba zaidi, hivyo kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure) na mtu kupata ugonjwa wa Mshtuko wa Moyo (Heart Attack). Mkusanyiko wa mafuta na pleteleti za damu wakati mwingine, huweza kumeguka katika mfumo wa mabonge na kusafiri kwenda kuziba mishipa midogo ya damu kichwani. Hali hii ikitokea, mtu hupata Kiharusi (Stroke/ Cerebrovascular Accident).

credits: GPL 

Comments

Popular posts from this blog

ULAJI WA VYAKULA HIVI UNAWEZA KUPELEKEA UTASA KWA ZAIDI YA 18%

MAKALA FUPI | BROZ MEDIA TZ Mwanamke ambaye ana mazoea ya kula vyakula vyenye mafuta mengi na sukari bila ya kutumia matunda kwa wingi, yumo kwenye hatari ya kutopata uja uzito, utafiti unasema . Utafiti uliofanyiwa wanawake 5,598, uliwapata wale ambao wana mazoea ya kula vyakula vyenye mafuta mengi, mara 4 au zaidi kwa wiki, wanachukua zaidi ya mwezi mmoja kupata uja uzito, kuliko wanawake ambao hawatumii kabisa chakula cha aina hiyo. Walaji wengi wa chakula cha aina hiyo, pia sio rahisi kupata mimba, katika kipindi cha mwaka mzima, hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya uzazi wa binadamu. Wataalamu wanasema kwamba, lishe bora huboresha uwezekano wa kushika mimba. Hata hivyo, kumekuwa na changamoto fulani na utafiti huo, ukiwemo swala la wanawake kujaribu kukumbuka, kile walichokuwa wa kila wakati wana uja uzito. Wanawake nchini Australia, New Zealand, Ireland na Uingereza, waliulizwa kuhusiana na kile walichokuwa wakila mwezi mmoja kabla ya kushika mimba, hasa...

Fahamu vyakula vinavyo weza sababisha mwanamke kuwahi kufikia ukomo wa hedhi

  Utafiti umebaini ulaji wa tambi na wali kwa wingi husababisha ukomo wa hedhi mapema Vyakula vyenye wanga kwa wingi husababisha wanawake kukoma hedhi mapema , utafiti umeeleza. Ulaji wa tambi na wali kwa wingi kwa wanawake nchini Uingereza kunasababisha kuwahi kukoma kwa hedhi mwaka mmoja na nusu mapema zaidi ya wastani wa umri wa miaka 51 . Hata hivyo, utafiti uliofanywa na Chuo kikuu cha Leeds kwa wanawake 914 nchini Uingereza , pia umebaini kuwa mlo ulio na mafuta ya samaki kwa wingi na njegere na maharage unaweza kuchelewesha ukomo wa hedhi kwa wanawake. Lakini wachambuzi wanasema kuna sababu nyingine, zikiwemo jenetiki Haijafahamika ni kwa ukubwa gani ulaji chakula unaweza kuleta athari kwa wanawake kama tafiti zinavyoeleza. Utafiti ulichapishwa kwenye jarida la Afya la Epidemiology & Community Health na wanawake waliulizwa mlo wao huwa una vyakula gani Mlo wenye mboga za jamii ya kunde kwa wingi, kama vile njegere,maharage,maharage membamba na...